Saudi Arabia yasema iko tayari kushirikiana na Tanzania uendelezaji wa reli ya SGR
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ameikaribisha Saudi Arabia kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali zikiwemo utalii, kilimo, madini, uendelezaji wa miundombinu pamoja na uchumi wa buluu.
Dkt. Nchemba ametoa mwaliko huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia, Eng. Ammar Naqadi, Kando ya Mkutano wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji, lililoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania, kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), lililofanyika hivi karibuni Mjini Riyadh nchini Saudi Arabia.
Amebainisha kuwa Tanzania inaendelea na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambapo imeshakamilika kipande kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na ujenzi unaendelea kwa vipande vinavyoelekea Mwanza na DRC kupitia Burundi hivyo ni fursa kwa Saudi Arabia kuwekeza katika miundombinu hiyo ambayo itachochea ukuaji wa bishara kati ya Saudi Arabia, Tanzania na nchi za Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchumi na Mipango wa Saudi Arabia, Eng. Ammar Naqadi, amesema Saudi Arabia iko tayari kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa miundombinu ya reli ili kurahisisha usafirishaji wa watu, mazao na mizigo ili kuchochochea ukuaji wa biashara ambapo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Amesema nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania katika fursa za kuendeleza sekta ya madini, kilimo, mafuta na gesi, utalii, uchakataji wa mazo ya bahari miundombinu pamoja na utalii ambapo wataandaa timu ya wataalamu kwa kushirikiana na Sekta binafsi kutembelea Tanzania kujionea fursa za uwekezaji katika sekta hizo, ili kujiridhisha na mazingira ya fursa za Tanzania ili kuweza kuwekeza.