Waziri Gwajima: Wasio na elimu ya uandaaji wa maudhui mtandaoni waache mara moja
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amekemea ongezeko la maudhui yasiyofaa yanayozalishwa na waandaji wa maudhui mtandaoni (content creators) na kuwataka kuzingatia weledi ili kuepuka uvunjifu wa maadili ya kijamii.
Dkt Gwajima amesema, hivi karibuni baadhi ya maudhui yasiyo na weledi na maadili ya Kitanzania yamesambazwa mtandaoni kama vile, kuuza figo za mtoto, kuandaa vinywaji na vyakula vichafu na kujitapa kwamba anawauzia wananchi wa Kariakoo, kufanya mapenzi hadharani na mapenzi ya jinsia moja pia kutangaza kuhusu fursa za kujipatia fedha kwa njia zisizoeleweka.
“Jamii ya Watanzania inastahili kujipambanua kwa heshima na kuheshimu makundi ya rika zote yanayofanya shughuli mbalimbali za haki humo mitandaoni ambapo yanastahili heshima na staha,” amesema Dkt Gwajima.
Aidha, Dkt Gwajima ametoa wito kwa waandaaji ambao hawana elimu na ufahamu kuhusu uandaaji maudhui mtandaoni kuacha mara moja, na maudhui ambayo yamekwisha pakiwa mtandaoni yaondolewe mara moja na kwamba wanaokiuka watawajibishwa kisheria.