Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Doto Maduhu Sita (32) mkazi wa Kishiri, Wilaya ya Nyamagana ambaye ni baba wa kambo wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi kwa tuhuma za kumbaka, kumlawiti na kumshambulia mtoto huyo.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema mtoto huyo alikuwa akifanyiwa ukatili huo mara kwa mara na kupelekea hali yake ya kiafya kuwa dhaifu, hivyo kuwafanya raia wema kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto.
“Kutokana na taarifa hizo, Polisi walifika eneo la tukio hilo na kumkuta mtuhumiwa huyo akishirikiana na mke wake aitwaye Aneth Mhano (23), wakiwa katika jitihada za kumpeleka mtoto huyo ili apate tiba,” imeeleza taarifa.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema katika harakati za matibabu katika Zahanati ya Serikali, Igoma mkoani humo, mtoto huyo alifariki dunia.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema mbali na kumshikilia mwanaume huyo, pia limemkamata mama mzazi wa mtoto huyo kwa kushindwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa majirani zake juu ya ukatili aliokuwa akifanyiwa mtoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa na kuokoa maisha ya mtoto.
Mwili wa mtoto huyo umekabidhiwa kwa baba yake mzazi aitwaye Emmanuel Daud (28) mkazi wa Maaduka Tisa, Wilaya ya Ilemela kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi.