Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limewaonya wananchi waliotaka kumshambulia mwananchi mmoja wakimtuhumu kuwa ni mbakaji maarufu kwa jina la ‘Teleza’.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema kumekuwa na uvumi wa taarifa potofu zinazoenezwa kwenye maeneo hususan Kata ya Mkolani na Buhongwa mkoani humo zikieleza juu ya mtu aitwaye Teleza anayedaiwa kubaka, kulawiti wanawake pamoja na kuwajeruhi.
“Jeshi la Polisi linalaani kitendo cha baadhi ya wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kutaka kumshambulia mwananchi eneo la Mtaa wa Ibanda, katika nyumba ya kulala wageni, Kata ya Mkolani, Wilaya ya Nyamagana, saa 4.00 usiku ambaye tulifanikiwa kuokoa maisha yake ambapo walimtuhumu kuwa ni Teleza na wakidai kwamba ndiye anaye wabaka na kulawiti wanawake wa maeneo hayo,” limesema Jeshi la Polisi.
Aidha, jeshi limesema taarifa hizo si za kweli bali ni za kufikirika, na kutokana na kitendo hicho, Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuhusika kutenda uhalifu huo ikiwemo wanaochapisha na kutoa taarifa potofu kwa wananchi, kwakuwa taarifa hizo zinaweza kuleta taharuki na uvunjifu wa amani.