Wanaume wawili waliovalia mavazi ya kike wauawa na Polisi katika tukio la ujambazi Mwanza

0
32

Watu wawili wa jinsia ya kiume wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa eneo la Kabambo, Kata ya Kiseke, Tarafa ya Ilemela mkoani Mwanza kwa kupigwa risasi na Askari polisi waliokuwa wakifanya doria eneo hilo baada ya kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara aitwaye Flora Sungura Abdallah (42) kwa lengo la kufanya uhalifu.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza imesema watu hao ambao majina yao na anuani zao hazikuweza kufahamika, walikuwa wamevalia mavazi ya kike ambayo ni gauni na vilemba kwa lengo la kuficha jinsia na muonekano wao, walifanikiwa kuingia ndani wakati mfanyabiashara huyo amefunguliwa geti wakati akitoka kwenye shughuli zake, ambapo walikuwa na bunduki aina ya shortgun moja iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi mbili na mapanga mawili.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa baada ya watu hao kuingia, wakazi wa eneo hilo walipiga kelele za kuomba msaada na ndipo taarifa hizo ziliwafikia polisi. Baada ya polisi kufika waliwataka watu hao kujisalimisha lakini walikaidi amri hiyo na kutaka kuwadhuru wakazi wa nyumba hiyo pamoja na askari.

“Askari wa Jeshi la Polisi walifyatua risasi na hivyo kusababisha watu wawili ambao mmoja alishika bunduki na mwingine akiwa na panga kujeruhiwa kwa risasi hizo, na kusababisha kupoteza maisha papo hapo. Miili ya watu hao ambayo hata hivyo haijatambuliwa imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Bugando ikisubiri utaratibu wa utambuzi na uchunguzi wa kitaalam (Post mortem) katika tukio hilo hakuna mali iliyoibiwa,” imesema taarifa.

Aidha, taarifa imeeleza kuwa katika tukio hilo watu wawili jinsia ya kiume ambao walikuwa ni washiriki katika tukio hilo walifanikiwa kutoroka kwa kutumia usafiri wa pikipiki, na kwamba msako mkali unaendelea ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.