Watatu washikiliwa kwa mauaji ya watu wawili kisa mgogoro wa ardhi

0
16

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu watatu, Kuva Zengo (25), Lukeresha Mlawa (32) na Bulanda Mathias (25) wote wakiwa wakazi wa Kijiji cha Luhanga kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili, Oddington Mjengwa (38) na Maige Jifaru (44) pamoja na kuwajeruhi wengine watano huko Wilaya ya Mbarari mkoani Mbeya chanzo kikiwa ni mgogoro wa ardhi.

Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema Januari 10, 2025 jioni katika Kijiji na Kata ya Luhanga ulitokea ugomvi baina ya familia mbili ya Mzee Rafael Mjengwa dhidi ya familia ya Mzee Malewa ukihusu shamba lenye ukubwa wa ekari 1050, ambapo familia ya Mzee Malewa pia wanadai shamba hilo ni la familia yao kwani wamekuwa wakilitumia kwa muda mrefu.

“Familia ya Mzee Rafael wakiwa wanaendelea na maandalizi ya kilimo katika shamba hilo, ghafla walishambuliwa na kundi la watu wapatao 15 wanaodaiwa kuwa ni wa Mzee Malewa na kusababisha watu wawili kufariki dunia na wengine watano kujeruhiwa,” imesema.

Jeshi la Polisi limesema baada ya ufuatiliaji limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni miongoni mwa watuhumiwa 15 waliotekeleza tukio hilo.

Send this to a friend