Burkina Faso yapiga marufuku majaji kuvaa mawigi ya kikoloni mahakamani
Kiongozi wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré amepiga marufuku majaji kuvaa mawigi yanayofanana na mitindo ya kikoloni ya Uingereza na Ufaransa, ikiwa ni juhudi za kuondoa athari za ukoloni kwenye mfumo wa mahakama wa taifa hilo.
Katika tangazo lake, Rais Traoré amesisitiza umuhimu wa kuachana na desturi za kikoloni na badala yake kukumbatia desturi za nchi hiyo na kukuza utambulisho wa nchi ya Burkina Faso, kwani mawigi ya enzi za ukoloni yamekuwa yakionekana kama alama za ushawishi wa kigeni katika mifumo ya kisheria ya Afrika.
Mawigi hayo yalianzishwa na wakoloni kama sehemu ya mavazi rasmi ya mahakama ili kuashiria mamlaka, utulivu, na heshima na baada ya ukoloni kumalizika, baadhi ya nchi za Afrika zimeendeleza matumizi ya mawigi hayo katika mifumo yao ya kisheria.