Wizara ya Fedha imewatahadharisha wastaafu wote nchini kuwa makini na ujumbe mfupi uliozuka hivi karibuni unaotumwa wa kitapeli, ukionesha mtu aliyetumiwa ujumbe alipigiwa simu na Hazina na hakupatikana, na anahitajika kufika Ofisi za Hazina Ndogo huku ukimtaka apige simu kwa namba zilizoandikwa kwenye ujumbe kwa maelezo zaidi.
Wizara imeutaarifu umma kuwa hakuna zoezi lolote la uhakiki wa mafao linalofanywa na Hazina na huduma za wastaafu hutolewa bure pasipo malipo na pia imesema Hazina haitumi ujumbe mfuoi kwa njia ya simu ya mkononi kwa wastaafu.
“Wizara ya Feedha inasisitiza kuwa mwananchi yeyote apatapo ujumbe huo apuuze na atoe taarifa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba 15040 au Kituo cha Polisi kilicho karibu naye,” imesema taarifa.
Wizara imesema mstaafu yeyote mwenye maswali na maoni anashauriwa kufika Ofisi za Hazina Ndogo iliyopo mkoani kwake.