Mjue Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mgombea Mweza wa Urais

0
3

Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya.

Alisoma Shule ya Msingi Oysterbay jijini Dar es Salaam kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1986.

Alijiunga Shule ya Sekondari Uru kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Tatu mwaka 1987 hadi 1989, na kisha alijiunga Shule ya Sekondari Sangu ambapo alisoma kidato cha Nne mwaka 1990.

Kidato cha Tano na Sita alisoma shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya na baadaye alijiunga na Chuo cha IDM Mzumbe mkoani Morogoro ambapo alihitimu mwaka 1997.

Wakati anahitumu mwaka 1997, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Mwaka 1998, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Dkt. Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 hadi 2003.

Pia alisoma shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 hadi mwaka 2003.

Mwaka 2003 hadi 2005 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Alifanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2011.

Mwaka 2005 alishinda Ubunge wa jimbo la Songea Mjini, na baadaye akateuliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo.

Pia aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, na kuhamishiwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, na baadaye Naibu Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi 2010.

Dkt. Nchimbi alihudumu kama Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo hadi Mei 2012.

Baadaye akawa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu mwaka 2013.

Desemba 2016, Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimteua Dkt. Nchimbi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, kisha Rais Samia Suluhu alimteua kuwa Balozi wa Misri kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka 2023.

Mnamo Januari 15, 2024 Dkt. Nchimbi aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi.

Januari 19, 2025, kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan alimpendekeza Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mweza wa Urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.