Noti zenye saini ya Dkt. Mwigulu Nchemba kuingizwa kwenye mzunguko kuanzia Februari

0
6

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emanuel Tutuba amesema noti mpya za Tanzania zenye saini ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia Februari mosi mwaka huu.

Gavana Tutuba amesema hayo wakati akimkabidhi Dkt. Nchemba, noti kifani za shilingi elfu kumi, elfu tano, elfu mbili na Shilingi elfu moja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.

“Mheshimiwa Waziri, ninayofuraha kukujulisha kuwa zoezi letu la uchapaji upya wa Noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la Serikali,” amesema Tutuba.

Gavana Tutuba amefafanua kuwa noti hizo zitatumika sambamba na noti zilizopo hivi sasa, zina mwonekano wa noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Emmanuel Tutuba,” ameongeza.

Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.