Mwanaume anayejulikana kwa jina la John Kiama Wambua anashikiliwa na polisi nchini Kenya kwa tuhuma za kumuua kikatili mke wake, Joy Fridah Munani, mwenye umri wa miaka 19.
Wambua mwenye umri wa miaka 29, alikamatwa mapema Jumanne asubuhi katika eneo la Huruma, Nairobi, akiwa na begi lililokuwa na sehemu za mwili wa binadamu.
Kulingana na afisa wa uchunguzi, wakati wa mahojiano, mshukiwa aliwaongoza polisi hadi nyumbani kwake, ambapo sehemu nyingine za mwili wa binadamu zilipatikana zikiwa zimefichwa chini ya kitanda. Wambua alikiri kuwa mabaki hayo ni ya mke wake, Joy Fridah.
Taarifa zinaeleza kuwa mshukiwa alifanya kitendo hicho baada ya mzozo uliotokea alipomkuta mke wake akiwa na mwanaume mwingine. Pia alikiri kukata mwili wa marehemu katika jaribio la kuuficha.
Polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Huruma wakishirikiana na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walifanya uchunguzi wa eneo la tukio na wakapata moja ya silaha zinazodaiwa kutumika katika mauaji hayo.
Mahakama imeamuru polisi kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa siku 21 ili kukamilisha uchunguzi.