Mganga Mkuu wa Serikali: Tusizushe taharuki juu ya ugonjwa wa Marburg

0
8

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Grace Magembe amewataka wananchi hususan wa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kutozusha taharuki na hofu na badala yake kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Marburg ambao kwa kiasi kikubwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta imeudhibiti.

Amesema hayo alipofika wilayani Biharamulo kwa ziara ya kikazi ikiwa ni pamoja na kuwatembelea wahisiwa wa ugonjwa huo ambao wamewekwa karantini, huku wakiendelea kupatiwa vipimo, Dkt. Magembe amesema licha ya kuendelea kuchukua tahadhari shughuli za uchumi lazima ziendelee kama kawaida.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema pindi wanapoona dalili zisizo za kawaida huku akitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa hizo.

Kuhusu tahadhari za Afya mahali pa kazi, Dkt. Magembe ametoa wito kwa watumishi wa Afya kuvaa mavazi maalum katika kujikinga na ugonjwa huo, huku pia akitoa wito kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa, dini na kimila kutoa elimu namna ya kujikinga na Marburg.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema suala la elimu na hamasa limekuwa likiendelea nyumba kwa nyumba ambapo wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamekuwa na mchango mkubwa.