Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia zimetenga dola bilioni 40 za Kimarekani [TZS trilioni 102] ili kufikia lengo la kufanikisha upatikanaji wa huduma kwa watu milioni 300 barani Afrika.
Akizungumza Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinumwi Adesina katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Kiafrika kuhusu Nishati ulioanza hapo jana Januari 27, 2025 katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam, amesema kati ya fedha hizo, dola bilioni 18.2 [TZS trilioni 45.9] ni kutoka AfDB na dola bilioni 22 [TZS trilioni 55.5] ni kutoka Benki ya Dunia.
“Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia zimetengeneza njia iliyo wazi kabisa ya kufikia lengo la upatikanaji wa huduma kwa watu milioni 300. Pamoja, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia zitatoa dola bilioni 40 [TZS trilioni 102] kufanikisha lengo hilo,” amesema.
Ameongeza kuwa “Jitihada zetu za pamoja ni kuwasaidia ninyi, wakuu wa nchi na serikali, kuendeleza na kutekeleza hatua madhubuti zilizoainishwa katika mikataba ya kitaifa ya nishati inayosimamiwa na nchi husika, ambayo ni ahadi yenu ya kutimiza maono yenu ya upatikanaji wa umeme katika nchi zenu.”
Naye, Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga amesema ili kufanikisha lengo la kufikisha huduma ya umeme wa bei nafuu kwa watu milioni 300 Afrika, ni lazima kuwepo na ushirikiano kati ya Serikali pamoja na sekta binafsi ili kuvutia uwekezaji binafsi, na kutoa umeme wa kuaminika na endelevu.
“Hii itahitaji nia ya kisiasa, uvumilivu, na maono ya muda mrefu. Serikali zitahitaji pia msaada wa kukidhi malengo haya ya miundombinu, na hapo ndipo IMF, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, na washirika wetu wengine wanapoweza kusaidia kwa kusaidia kutoa rasilimali,” ameeleza.