Ubalozi wa Kenya nchini DRC wavamiwa na waandamanaji

0
25

Ubalozi wa Kenya uliopo Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umeshambuliwa na waandamanaji wenye hasira wakipinga mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Kenya, Korir Sing’oei ameielezea hali hiyo kama kitendo cha ghasia kilichofanywa na waandamanaji waliokuwa wakionesha kutoridhishwa kwao na hali ya usalama mashariki mwa DRC.

Waandamanaji hao walilenga balozi za nchi wanazozituhumu kushirikiana na Rwanda katika kuunga mkono waasi wa M23 ambao wameuteka mji mkuu wa jimbo la mashariki, Goma ukiwemo ubalozi wa Kenya, Rwanda, Uganda, Ufaransa na Marekani.

Mashambulizi hayo yamekuja wakati ambapo mapigano makali yanaendelea kati ya waasi wa M23 ambao wanashutumiwa kuungwa mkono na Rwanda, na majeshi ya serikali ya Congo, yakisaidiwa na wanamgambo wanaounga mkono serikali.

Mapigano hayo yameleta madhara makubwa, huku watu 17 wakiripotiwa kuuawa na miili mingi ikiachwa barabarani. Hospitali katika maeneo hayo zimeelemewa na idadi kubwa ya majeruhi.

Rais wa DRC, Félix Tshisekedi hapo jana aliitisha mkutano wa dharura akishirikiana na viongozi wa kitaifa, ili kujadili hali inayozidi kuwa mbaya mashariki mwa nchi hiyo.

 

Send this to a friend