Mwanamke mmoja kutoka mji wa Sindo, Suba Kusini, Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya, ameuawa na kundi la watu wenye hasira kali kwa kupigwa hadi kufa baada ya kudaiwa kuiba mtoto wa mwaka mmoja na nusu.
Marehemu, aliyefahamika kwa jina Jane Atieno, alikumbana na ghadhabu ya umati baada ya kudaiwa kuiba mtoto huyo na kumkabidhi kwa mwendesha pikipiki ili atoroke naye.
Inaripotiwa kuwa alifanya tukio hilo alipokwenda nyumbani kwa mama wa mtoto huyo kwa ajili ya kununua kuni za kupikia.
Mama wa mtoto aligundua baadaye kuwa mtoto wake ametoweka, na alipomuuliza Jane kuhusu alipo, alidai hakumwona, hali iliyomfanya mama huyo kupiga yowe akiomba msaada kutoka kwa wananchi, ambao walimvamia Jane na silaha za jadi.
Marehemu alikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Suba kwa matibabu lakini alifariki dunia akiwa hospitalini.