Elon Musk: USAID ni shirika la kihalifu, linapaswa kufungwa
Mmiliki wa kampuni ya teknolojia, Elon Musk ametangaza kuwa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) linapaswa kufa kwakuwa ni shirika la kihalifu.
Musk, ambaye aliteuliwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kuongoza Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE), ametoa kauli hiyo baada ya maafisa wawili kutoka USAID kujaribu kuwazuia wafanyakazi wa Idara ya Musk kuingia kwenye mifumo ya usalama ya USAID.
Kulingana na vyanzo vya habari, mifumo ya USAID ambayo timu ya DOGE ilijaribu kuifikia ilijumuisha faili za wafanyakazi na mifumo ya usalama, ikiwemo mifumo ya siri zaidi ya kiwango cha usalama cha baadhi ya wafanyakazi wa DOGE.
USAID ilianzishwa mwaka 1961 na kwa muda mrefu limekuwa shirika kuu la serikali ya shirikisho linalotoa misaada ya kigeni. Hata hivyo, ripoti kadhaa zimeonesha kuwa Rais Donald Trump sasa anajaribu kulifunga shirika hilo kama taasisi huru na kuhamishia shughuli zake chini ya Wizara ya Mambo ya Nje.