Kwanini Trump na Musk wanalipinga shirika la misaada la USAID?

0
17

Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) limekuwa sehemu muhimu ya sera za misaada ya nje ya Marekani kwa zaidi ya miaka 60. Hata hivyo, chini ya utawala wa Rais Donald Trump, na kwa ushawishi wa Elon Musk, USAID linakumbwa na shinikizo kubwa la kufutwa au kufanyiwa mabadiliko makubwa.

Shirika hili linafanya kazi zaidi ya nchi 100, likijikita katika afya ya kimataifa, ukuaji wa uchumi, majanga, na kuimarisha demokrasia.

Hata hivyo, mnamo Januari 20, 2025, Rais Trump alisaini Amri ya Utendaji 14169 iliyopewa jina ‘Tathmini na Urekebishaji wa Misaada ya Kimataifa ya Marekani.’ Amri hiyo iliweka zuio la siku 90 kwa programu zote za misaada ya maendeleo ya Marekani, likilenga kutathmini ufanisi wa misaada hiyo na iwapo inaendana na maslahi ya taifa.

Hatua hiyo imesababisha kusitishwa kwa miradi mingi ya misaada duniani, kufutwa kazi kwa wafanyakazi wa shirika, na kusababisha athari kubwa katika sekta za afya, usalama wa chakula, na elimu katika maeneo yaliyo hatarini.

Lakini kwa nini Marekani, hasa Trump na Musk, wanapinga USAID? Na nini athari zake hasa kwa nchi za Afrika?

Kudaiwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha

Trump na Musk wanadai kuwa USAID limekuwa likitumia mabilioni ya dola kwa miradi ya kimataifa isiyo na uwazi wa matumizi na inayonufaisha mashirika ya nje badala ya raia wa Marekani.

Kudhoofisha maslahi ya Marekani

Utawala wa Trump umedai kuwa USAID limekuwa likifadhili miradi ambayo haina manufaa ya moja kwa moja kwa Marekani na badala yake linatumika kuendeleza sera zisizoendana na sera za Marekani. Trump amesisitiza kuwa rasilimali za Marekani zinapaswa kuelekezwa kwa wananchi wake kwanza badala ya kusaidia mataifa ya nje.

Ushindani wa kisiasa na kiuchumi

Musk, kama mfanyabiashara mkubwa, anaamini kuwa misaada ya kimaendeleo inapaswa kufanywa kwa njia ya uwekezaji wa moja kwa moja badala ya misaada ya bure. Hii inalingana na sera za utawala wa Trump, ambao unataka kupunguza misaada ya kimataifa na badala yake kushawishi biashara na uwekezaji wa sekta binafsi.

Masuala ya usalama na udhibiti wa taarifa

Hivi karibuni, kumekuwa na mvutano kati ya USAID na Kitengo cha Ufanisi wa Serikali (DOGE) kinachoongozwa na Elon Musk. Wafanyakazi wa DOGE walidaiwa kushinikiza kupata nyaraka za siri za USAID, jambo lililosababisha kuondolewa kazini kwa maafisa wawili waandamizi wa usalama wa shirika hilo. Hii inaonyesha kuwa upinzani dhidi ya USAID unaweza pia kuwa na mwelekeo wa kiusalama na udhibiti wa taarifa.

Athari za kufutwa kwa USAID kwa Afrika

Kupungua kwa misaada ya kimaendeleo

Mataifa mengi ya Afrika yanategemea USAID kwa misaada ya maendeleo, ikiwemo miradi ya afya, elimu, na kilimo. Kupungua au kukomeshwa kwa misaada hiyo kunaweza kusababisha kuzorota kwa huduma za kijamii katika mataifa mengi barani Afrika.

Kudhoofika kwa Sekta ya Afya

USAID imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa sekta ya afya barani Afrika, hasa katika mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria, na magonjwa mengine ya kuambukiza. Endapo misaada hii itasitishwa, maisha ya mamilioni ya watu yatakuwa hatarini kutokana na uhaba wa dawa na vifaa vya matibabu.

Kudhoofika kwa ustawi wa kilimo

Miradi mingi ya USAID inahusiana na kusaidia wakulima wadogo kwa kuwapatia mbegu bora, mbolea, na mafunzo ya kisasa ya kilimo. Kusitishwa kwa misaada hii kunaweza kuathiri usalama wa chakula katika mataifa yanayokabiliwa na changamoto za ukame na uhaba wa chakula.

Kuchochea ushawishi wa mataifa pinzani

Ikiwa Marekani itajiondoa katika kusaidia mataifa ya Afrika, kuna uwezekano mkubwa kwamba mataifa kama China na Urusi yataongeza ushawishi wao barani humo. Hii inaweza kubadili uwiano wa kisiasa na kiuchumi, huku mataifa ya Afrika yakigeukia nchi hizo kwa msaada wa maendeleo.

Kwa sasa, hatima ya USAID haijulikani. Wafuasi wa shirika hilo wanatoa wito kwa bunge la Marekani kuingilia kati ili kulinda programu zake, wakisisitiza kuwa misaada ya kimataifa ni muhimu si tu kwa masuala ya kibinadamu bali pia kwa maslahi ya kimkakati ya Marekani duniani.