Ripoti ya Kifedha ya Exim Bank 2024 Yaonesha Mafanikio Makubwa na Ubunifu wa Kifedha

0
5

Dar es Salaam, Tanzania: Benki ya Exim Tanzania imetoa ripoti yake yenye matokeo mazuri ya kifedha kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2024, ikionesha ukuaji mkubwa katika viashiria muhimu vya kifedha na kama taasisi. Jumla ya mali za benki hiyo zimeongezeka kwa 4.7%, kufikia TZS trilioni 3.1, na kuimarisha nafasi yake kama mojawapo ya taasisi zinazoongoza katika sekta ya kifedha Tanzania. Kiasi cha mikopo yake kimefikia TZS trilioni 1.8, ikirekodi ongezeko la kuvutia la 19.1% kwa mwaka.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu, alisema, “Matokeo yetu ya 2024 yanaonesha dhamira yetu ya ukuaji endelevu na ujumuishaji wa kifedha. Tumewekeza kimkakati katika mageuzi ya kidijitali, huduma za kibenki zinazomlenga mteja, na upanuzi wa kikanda, kuhakikisha kuwa tunasalia mstari wa mbele katika ubunifu na ubora wa huduma.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu (katikati), akizungumza na wanahabari wakati wa kutangaza Ripoti ya Fedha ya 2024 ya benki hiyo, ikionesha mafanikio makubwa ya kifedha na ukuaji endelevu. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Rejareja, Andrew Lyimo, na Afisa Mkuu wa Fedha, Shani Kinswaga (kulia), katika hafla iliyofanyika hivi karibuni katika Makao Makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam.

Faida ya benki kabla ya kodi ilifikia TZS bilioni 139.7, ikiwa na ongezeko la asilimia 52.7 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku faida baada ya kodi ikiwa TZS bilioni 90, ambayo inadhihirisha ongezeko la asilimia 48.8. ” Utendaji huu wa kipekee ni matokeo ya maboresho katika operesheni zetu, uwekezaji wa kimkakati, na juhudi zetu za kuendelea kuwapatia wateja wetu huduma bora”.Tunashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini na kutuunga mkono, jambo ambalo limekuwa muhimu katika kufikia matokeo haya. “Pia, mazingira bora ya biashara yamechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza ukuaji, na kutuwezesha kuchukua fursa zinazoendana na malengo yetu ya muda mrefu.” amesema Mkurugenzi wa Fedha wa benki, Shani Kinswaga.

Ukuaji huu unatokana na dhamira ya benki hiyo ya kusaidia wafanyabiashara na watu binafsi kwa kutoa huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji yao, huku ikizingatia usimamizi bora wa mali. Kwa mantiki hiyo, kiwango cha mikopo isiyolipwa kimesalia chini ya kiwango cha udhibiti kwa 2.7% kufikia 31 Desemba 2024. Uwekaji wa fedha kwa wateja ziliongezeka hadi TZS trilioni 2.5, ongezeko la 4.2%, ikiashiria imani ya wateja na ufanisi wa bidhaa za kifedha za Exim Bank katika kukidhi mahitaji mbalimbali ya kibenki.

Afisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Shani Kinswaga, alisisitiza uimara wa kifedha wa taasisi hiyo: “Matokeo yetu yanaonesha mfumo madhubuti wa usimamizi wa hatari na ufanisi wa uendeshaji. Ukuaji mkubwa wa mtaji wa wanahisa, ambao umeongezeka kwa 32.6% hadi TZS bilioni 412.2, unathibitisha dhamira yetu ya muda mrefu ya kutoa thamani kwa wadau wetu.”

Mapato yasiyotokana na riba, ambayo ni sehemu muhimu ya utofauti wa mapato, yaliongezeka kwa 20.1% hadi TZS bilioni 123.7. Ukuaji huu unaonesha mkakati wa benki wa kupanua huduma za kibenki za kidijitali na vyanzo mbadala vya mapato, unaochochewa na maboresho endelevu ya huduma kwa wateja kupitia mifumo salama na rahisi ya kidijitali.

Andrew Lyimo, Mkuu wa Huduma za Rejareja wa Exim Bank, alisisitiza umuhimu wa benki ya kidijitali katika kukuza ujumuishaji wa kifedha: “Tunaendelea kupanua mfumo wetu wa kibenki wa kidijitali, tukitoa huduma za kifedha salama na rahisi kwa watu binafsi na wafanyabiashara. Kipaumbele chetu ni kutumia teknolojia kuboresha uzoefu wa wateja na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kote nchini.”

Inapoangazia mbele, Exim Bank inaendelea kujidhatiti kuimarisha nafasi yake kubwa kupitia ubunifu endelevu, ushirikiano wa kimkakati, na upanuzi wa mtandao wake kikanda. Dira ya benki hiyo kwa 2025 inajumuisha kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, kuhamasisha uwezeshaji wa kiuchumi, na kuendelea kuongoza katika huduma za kibenki za kidijitali. Kwa msingi thabiti na mkakati wa kisasa, Exim Bank iko tayari kwa mafanikio endelevu katika mazingira ya kifedha yanayoendelea kubadilika.

Akihitimisha ripoti hiyo, Bw. Matundu alisisitiza maono ya muda mrefu ya benki hiyo: “Matokeo haya ni ushuhuda wa dhamira yetu ya kuendeleza huduma za kifedha, ubunifu, na ukuaji unaomlenga mteja. Tunapoangalia mbele, kipaumbele chetu kitasalia katika kuongeza uwezo wetu wa kidijitali, kuimarisha upanuzi wetu kikanda, na kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kote nchini. Tumejizatiti kuunda mustakabali wa benki ndani na nje ya Tanzania.”