Trump asema Marekani itaichukua na kuimilika Gaza baada ya kuwaondoa Wapalestina

0
4

Rais Donald Trump amesema Marekani itachukua na kumiliki Ukanda wa Gaza baada ya kuwahamisha Wapalestina kwenda maeneo mengine, chini ya mpango wa maendeleo ambao unaweza kugeuza eneo hilo kuwa Riviera ya Mashariki ya Kati.

Akiznungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Trump amesema utawala wake utaongoza maendeleo katika Ukanda huo ili  kutoa ajira na makazi yasiyo na kikomo kwa watu wa eneo hilo.

“Marekani itachukua Ukanda wa Gaza, na tutafanya kazi nzuri huko pia. Tutaimiliki,” amesema Trump  akiongeza kuwa utawala wake utachukua jukumu la kusafisha majengo yaliyoharibiwa na kuondoa mabomu ambayo hayajalipuka na silaha nyingine hatari.

Hata hivyo, nchi jirani kama Jordan na Misri zimelikataa wazo hilo, huku balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa akisisitiza kwamba “Nchi yetu ni nchi yetu.”

Kundi la Hamas ambalo linatawala Gaza, limelaani pendekezo hilo na kulielezea kama mpango wa kusababisha machafuko na mvutano katika eneo hilo.

Naye, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema wazo hilo linapaswa kuzingatiwa.