Wizara ya Afya yafafanua upatikanaji wa dawa za ARV

0
70

Wizara ya Afya imesema dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) haziuzwi na zipo za kutosha, hivyo watumiaji wa dawa hizo hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa hizo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya imesema imebaini uwepo wa taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vingine vya Habari zikielezea uhaba wa dawa hizo nchini.

“Taarifa hizo ni za upotoshaji na zimeleta hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha baadhi ya wagonjwa kuomba kupewa dawa za muda mrefu kwa ajili ya akiba, jambo ambalo si sahihi na linaweza kuathiri utunzaji na matumizi sahihi ya dawa,” imesema taarifa.

Imeongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuweka mikakati thabiti na stahiki ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.

Aidha, Wizara imetoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizo na kuendelea kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya ili kuzuia usugu wa vimelea vya magonjwa hayo dhidi ya dawa.