Wakuu wa Nchi EAC na SADC wasisitiza mazungumzo kurejesha amani DRC

0
7

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inaendelea kujitolea kusaidia juhudi zinazoendelea za kidiplomasia kumaliza mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao umesababisha machafuko makubwa na vifo vya raia.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC Unaofanyika Ikulu Dar es salaam, amesema Tanzania ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama mashariki mwa DRC kwani mzozo unaoendelea unaweka dosari kubwa katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

“Kama wanachama hai wa EAC na SADC, ni lazima tuendelee kuwa imara katika azma yetu ya kuwa na kanda zenye amani na uthabiti, huku nchi zetu zikiishi kwa mshikamano na maelewano. Kwa hivyo, ombi langu la dhati kwenu, ni kwamba tuungane katika juhudi zetu za kukomesha machafuko kwa kudumisha maendeleo na kuunda mazingira salama ambapo amani, usalama na maendeleo vinaweza kustawi,” amesema.

Naye, Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), William Ruto ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro huo, kusitisha mapigano mara moja na kuanza mazungumzo ya amani.

“Tunaliomba kundi la M23 kusitisha mashambulizi na jeshi la DRC kuepuka hatua za kulipiza kisasi. Ni kupitia kusitisha mapigano tu ndipo tutaweza kuanzisha mazungumzo yenye lengo la kurejesha amani, amesisitiza.

Ameongeza kuwa “Hali ya kibinadamu katika DRC ni mbaya sana. Mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao, na wengi wanakabiliwa na vitisho vya mara kwa mara vya vurugu, ikiwemo ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kuajiriwa kwa watoto kama askari. Ni wazi kuwa mgogoro huu ni mgumu na unahitaji juhudi za pamoja ili kuutatua.”

Rais Ruto amesema wakati wa kuchukua hatua ni sasa kwani imani ya mamilioni ya watu ipo kwa viongozi hao wakitegemewa kushughulikia hali hiyo kwa busara, huruma, na kujitoa kwa ajili ya amani na haki ya watu wa DRC.