Haya ndio maazimio ya Wakuu wa Nchi wa EAC na SADC kuhusu mzozo DRC

0
5

Katika jitihada za kurejesha amani na utulivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana katika Mkutano wa pamoja na kutoa mapendekezo na maamuzi muhimu kwa pande zote zinazohusika na mgogoro huo.

Mkutano huo umeonesha mshikamano wa mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika katika kusaka suluhisho la kudumu kwa mzozo ambao umeathiri maelfu ya raia wasiokuwa na hatia, huku wakitoa mapendekezo na maazimio kwa lengo kutoa suluhisho la mzozo huo.

Mapendekezo muhimu:

Usitishaji wa mapigano mara moja bila masharti yoyote:

Viongozi wa EAC na SADC wametaka kila upande unaohusika katika mgogoro wa DRC kusitisha mgogoro mara moja ili kuzuia madhara zaidi kwa raia na kuimarisha mazingira ya mazungumzo ya amani.

Ufunguzi wa Uwanja wa Ndege wa Goma:

Kufungwa kwa uwanja huo kumetatiza misaada ya kibinadamu na usafirishaji wa bidhaa muhimu. Mkutano huo umeagiza kufunguliwa mara moja kwa uwanja huo ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na utoaji wa misaada kwa wahanga wa mgogoro huo.

Urejeshaji wa miili ya marehemu na uokoaji wa majeruhi:
Mkutano umeagiza urejeshaji wa miili ya wale waliopoteza maisha kutokana na mapigano pamoja na kuweka utaratibu wa haraka wa kuwahudumia majeruhi.

Mazungumzo jumuishi kwa ajili ya suluhisho la kudumu:
Pande zote zimetakiwa kushiriki kwenye mazungumzo ya wazi na jumuishi, yakizingatia mchakato wa Nairobi na Luanda, ili kupata suluhu la kudumu kwa mgogoro wa DRC.

Kutokomeza vikundi vya waasi na kuondoa majeshi ya Rwanda:
Mkutano umehimiza hatua za haraka za kuangamiza vikundi vya waasi kama FDLR na kutaka kuondolewa kwa majeshi ya Rwanda katika ardhi ya DRC.

Kufunguliwa kwa njia kuu za usambazaji wa bidhaa:

Ili kupunguza athari za kiuchumi kwa raia, viongozi wameamuru kufunguliwa kwa barabara kuu za usafirishaji wa bidhaa na misaada ya kibinadamu, ikiwemo njia zinazounganisha Goma–Sake–Bukavu, Goma–Kibumba, Rutshuru, Bunagana, na safari za majini katika Ziwa Kivu kati ya Goma na Bukavu.

Kukomesha hotuba za chuki:
Viongozi wamezitaka pande zinazohusika na mgogoro kuepuka hotuba zinazochochea chuki na badala yake kujikita katika mazungumzo yenye lengo la kujenga amani ya kudumu.

Maazimio muhimu:
Mkutano umeelekeza wakuu wa majeshi wa EAC na SADC kukutana ndani ya siku tano ili kutoa mwelekeo wa kina kuhusu usitishaji wa vita, utoaji wa misaada ya kibinadamu, na kuhakikisha usalama katika mji wa Goma na maeneo jirani.

Serikali ya DRC imetakiwa kuhakikisha ulinzi wa balozi na ofisi za kidiplomasia zilizoko Kinshasa kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya ofisi hizo.
Pia, mataifa ya EAC na SADC yametakiwa kuendelea kushirikiana kidiplomasia na kisiasa ili kupata suluhu ya kudumu kwa mgogoro huo, badala ya kutegemea tu suluhisho la kijeshi.