Wakandarasi walipwa bilioni 254 kukamilisha miradi ya ujenzi
![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Snapinst.app_476559975_18050134907236473_2037959762933761582_n_1080-905x613.jpg)
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imelipa takribani TZS bilioni 254 ndani ya miezi miwili kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya barabara na madaraja nchini baada ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Ulega ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 inayojengwa kwa awamu mbili na wakandarasi wawili ambao ni CHICO pamoja na China First.
Waziri huyo amesema Rais Samia ametoa maelekezo ya kulipwa kwa wakandarasi hao, ili kuwajengea uwezo wa kukamilisha miradi yote ya sekta ya ujenzi kutekelezwa kama ilivyopangwa.
“Mmeona katika muda wa hii miezi mwili, Rais Samia tayari amelipa malipo ya wakandarasi ya takribani shilingi bilioni 254, matumaini yetu tunataka kuona kazi zikiendelea “, amesema Ulega.
Ulega ameongeza kuwa mwishoni mwa Februari mwaka huu, serikali inatarajia kutoa fedha nyingine za kutekeleza miradi ya miundombinu katika sekta ya ujenzi ambapo ameiagiza TANROADS kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ianze kujengwa haraka.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema barabara ya Ntyuka – Mvumi- Kikombo ni barabara ya kihistoria, hivyo ameomba Serikali kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni mkombozi kutokana na uwepo wa hospitali kubwa ya macho ya MVUMI inayotoa huduma nchi nzima na pia kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji hilo.