Serikali yakanusha kuingia makubaliano na mwekezaji uendeshaji Bandari ya Bagamoyo

0
19

Serikali imesema haijaingia makubaliano na mwekezaji yeyote kwa sasa kwa ajili ya kujenga na kuendesha Bandari ya Bagamoyo.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, imesema wakati wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa miradi mbalimbali iliyopo katika programu ya Ujenzi wa Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo (BSEZ), na wapo katika hatua mbalimbali za mazungumzo na taasisi mbalimbali za Serikali.

“Taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba kampuni moja kutoka Saudi Arabia imepata mkataba wa uwekezaji wa kujenga na kuendesha Bandari ya Bagamoyo sio za kweli,” imesema taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa “Kutokana na umuhimu na ukubwa wa programu ya BSEZ, umma utajulishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake.”

Aidha, taarifa hiyo imesema utekelezaji wa programu ya BSEZ, ambayo inahusisha ujenzi wa Bandari, Kongani za Viwanda, Kongani za TEHAMA, Ukanda huru wa Biashara na Kituo cha reli, utafanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali kupitia mpango wa Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP).

Send this to a friend