
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 26 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya upatu mtandaoni bila kuwa na kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 24, 2025, miongoni mwa waliokamatwa ni Najim Issa Houmud (34), Mkurugenzi Mkazi wa Kigamboni, Hatibu Kudura (25) Mkazi wa Kinondoni, Fatum Hamisi (26) Mkazi wa Kigamboni, na Athumani Sadik (29) Mkazi wa Mabibo.
Watuhumiwa hao walikamatwa kati ya Februari 18 na Februari 22, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya jiji, yakiwemo Mbagala, Gongolamboto, Tabata, Mbezi Magufuli, Ubungo Riverside, na Mabibo.
Jeshi la Polisi limesema kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania, walifanya uchunguzi wa kampuni ya Leo Burnett London (LBL), ambayo inadaiwa kuendesha biashara hiyo haramu ambapo uchunguzi ulibaini kuwa kampuni hiyo haina uongozi maalum na huwarubuni wananchi kujiunga kwa kulipa kiasi cha fedha kuanzia Shilingi 50,000.
“Na kuendelea ili kuwa wanachama pia huchangisha pesa kwa kuwadanganya wananchi kuwa watapata faida kubwa kwa muda mfupi bila ya wanachama kuhusishwa kwa namna yoyote katika shughuli za uendeshaji wa kampuni hiyo,” imesema taarifa.
Polisi wamesema kuwa uchunguzi bado unaendelea, na pindi utakapokamilika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa waangalifu na biashara za upatu mtandaoni, na kuhakikisha kuwa wanajiridhisha kabla ya kushiriki, kwani baadhi ya biashara hizo hazina leseni wala vibali vya kisheria.