
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) amesema nchi ya Tanzania imeendelea kuweka kipaumbele katika uendelezaji na ulinzi wa Haki za Binadamu kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Akizungumza wakati akiiwakilisha Nchi ya Tanzania katika Kikao cha 58 Cha Haki za Binadamu kinachofanyika Geneva nchini Uswisi , Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania imeendelea kusimamia utu wa kibinadamu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na inaendana na mkakati uliopitishwa na Rais Samia Suluhu ambao umejikita katika 4Rs, ambazo ni Maridhiano, Uthabiti, Mageuzi na Kujenga upya.
Akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa Haki za Binadamu katika Hifadhi ya Ngorongoro, Waziri Ndumbaro amesema kuwa Serika ya Tanzania imeendelea kuweka uwiano sawa wa haki za binadamu na maisha kwa kuzingatia uhifadhi.
Waziri Ndumbaro amefafanua kuwa Rais wa Tanzania katika kusimami Haki za Binadamu Ngorongoro, alikutana na viongozi wa Vijiji na Kimila na kusikiliza kero zao na kuanzisha tume mbili za ushauri, kushauri masuala ya ardhi na kushauri kuhusu mpango unaoendelea wa kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro kwenda Msomera.
Aidha, Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa lengo la jitihada hizo ni kuhakikisha zoezi la kuhama kwa hiari linafanya kazi kwa urahisi na kwamba kero za wananchi zinashughulikiwa.
Maeneo mengine ya usimamizi wa Haki za Binadamu yaliyowasilishwa katika Mkutano huo ni pamoja na kufanya Uchaguzi Huru na Haki kila baada ya miaka mitano, Uhuru wa Vyombo vya Habari na kujieleza, kulinda Haki za makundi hatarishi ukiwemo ustawi wa watu wenye ualbino na usaidizi kwa watu wenye ulemavu.