
Mwalimu mmoja katika Kaunti ya Nyamira nchini Kenya amelazwa katika hospitali ya Ikonge baada ya kushambuliwa na mwalimu mkuu kwa madai ya kuchelewa kufika shuleni.
Mwalimu huyo wa Sekondari aitwaye Vincent Onyancha amesema alifanyiwa vurugu mbele ya wanafunzi wake darasani wakati akifundisha ambapo mkuu huyo alimpiga makofi na kumpiga mateke.
“Niliwasili shuleni nikiwa nimechelewa kidogo, kisha mwalimu mkuu aliingia darasani na kunipiga nikiwa nafundisha. Alinipiga teke, makofi na kuniburuta hadi ofisini kwake ambako aliendelea kunipiga,” amesema Onyancha.
Maafisa wa Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari (KUPPET) wamelaani tukio hilo na kuitaka Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwalimu mkuu huyo.
Chama hicho kimeongeza kuwa iwapo hatua za kisheria hazitachukuliwa dhidi ya mwalimu mkuu huyo, walimu watalazimika kugoma ili kulalamikia ukatili huo.
Mkurugenzi wa TSC katika Kaunti ya Nyamira, Erick Magak, amethibitisha kupokea malalamiko hayo na kusema kuwa uchunguzi umekwishaanza.