
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mwanga, Lembrus Mchome, amemuomba Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika kujibu barua yake ya malalamiko ya kupinga uteuzi wa viongozi nane wa CHADEMA walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Akizungumza na vyombo vya Habari jijini Arusha, Mchome amesema kuwa akidi ya Baraza Kuu la CHADEMA wajumbe wake ni wanachama 412 na kwamba akidi inayotakiwa angalau iwe na wajumbe 309 sawa na asilimia 75, lakini viongozi hao walipitishwa na akidi ya wanachama 85 tu sawa na asilimia 20.6.
Mchome amesema mnamo Februari 18, mwaka huu aliwasilisha barua yake yenye kumbukumbu namba KM/CDM/AD/2025 kwa Katibu Mkuu, John Mnyika akitaka ufafanuzi wa uhalali wa viongozi hao kupitishwa na akidi ndogo ya wajumbe Januari 22, mwaka huu.
Miongoni mwa viongozi anaopinga uteuzi wao ni pamoja na Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar pamoja na wajumbe watano wa Kamati Kuu akiwemo Godbless Lema, akidai uteuzi wa viongozi hao ulikiuka katiba ya chama.
Hata hivyo, Mchome amempa siku mbili Katibu wa chama hicho ili kujibu malalamiko hayo kabla ya kwenda kwenye ngazi nyingine.