Ahitimu na kupata ‘scholarship’ chuo kikuu akiwa hajui kusoma wala kuandika

0
5

Aleysha Ortiz (19) kutoka nchini Marekani ameishitaki Bodi ya Elimu ya Hartford na mmoja wa walimu wake kwa uzembe, akidai kuwa hawezi kusoma wala kuandika, licha ya kuomba rasilimali za kielimu na msaada kwa miaka mingi bila mafanikio.

Aleysha amehitimu kwa heshima mwezi Juni kutoka shule ya upili na kupata udhamini wa masomo kwa chuo kikuu, lakini amesema hana uwezo wa kusoma wala kuandika baada ya kusoma kwa miaka 12.

Aleysha anasema walimu wake walikuwa wakimhamisha tu kutoka darasa moja hadi lingine katika shule ya msingi na sekondari. Lakini alipofika shule ya upili (high school), alijua jinsi ya kutumia teknolojia kutimiza kazi zake za darasani.

Aleysha amesema alikua akirekodi masomo yake yote kwa simu yake, kisha baadaye kusikiliza kila walichokisema walimu wake. Alitumia zana ya sauti kuyageuza maandishi kwenye kompyuta yake na kutafuta maana ya kila neno, kisha kugeuza maandishi kuwa sauti ambayo aliweza kuelewa. Mara alipoelewa kazi ya darasani, alijibu kwa sauti ambapo yaligeuzwa kuwa maandishi na kisha akaweka maneno hayo kwenye kazi yake ya nyumbani.

Kwa sababu ya msamiati wake mdogo na shida ya usemi, Aleysha anasema tafsiri haikuwa sahihi kila wakati au ilikuwa na makosa ya kisarufi. Hata hivyo, anasema matumizi ya teknolojia yalimsaidia kuinua alama zake kutoka C na D hadi A na B.

Amesema huanza kufanya kazi zake za shule mara tu alipokuwa akifika nyumbani kutoka shule na kumaliza kila siku saa saba au nane usiku kabla ya kuamka saa 12 asubuhi na kuchukua basi kwenda shuleni.

Hata hivyo, baada ya kufichua kuwa atajiunga na Chuo Kikuu cha Connecticut, Ortiz alifanyiwa vipimo vya ziada vilivyoonyesha kuwa ana tatizo la kusoma (dyslexia).