
Wizara ya Katiba na sheria imetuma Mawakili wa serikali takribani 50 ambao kwa siku nane mfululizo watakuwa mkoani Arusha, kusikiliza na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wa mkoa huo kupitia kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayokwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Mwanamke duniani inayofanyika Kitaifa mkoani Arusha, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu kwenye kilele chake Machi 08, 2025.
Moses Matiko, Wakili na mhadhiri msaidizi Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino, Kampasi ya Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa huduma za msaada wa kisheria kwa Mkoa wa Arusha ameeleza kuwa kupitia wizara watahakikisha kuwa wote wenye migogoro wanatatuliwa migogoro yao pamoja na kutoa msaada wa mawakili kwa wananchi ambao tayari walishafungua ama kufunguliwa kesi kwenye mahakama za ngazi mbalimbali.
Matiko amewaambia wanahabari Jijini Arusha kuwa kufanyika kwa kampeni hiyo kote Tanzania ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alibaini uwepo wa migogoro mingi ya kijamii na inayoweza kutatuliwa kwenye ngazi ya kijamii, mingi ikihusu mirathi, ndoa, utawala bora, ukatili wa kijinsia, matunzo kwa watoto pamoja na migogoro ya ajira na mahusiano kazini.
Kando ya uwepo wa mawakili wa serikali na wadau wengine wa sheria, kampeni hiyo pia inahusisha sekta binafsi ambapo kwa Mkoa wa Arusha kuna uwepo wa Mawakili kutoka kwenye Chama cha wanasheria wa Tanganyika TLS.