
Kiongozi wa jeshi la Gabon, Jenerali Brice Oligui Nguema, ametangaza nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi ujao, akisema uamuzi huo ni baada ya maombi mengi kutoka kwa wananchi.
Nguema alichukua madaraka mwaka 2023 kupitia mapinduzi yaliyoangusha utawala wa muda mrefu wa familia ya Bongo, ambapo baada ya kuchukua madaraka, aliahidi kuwakabidhi raia mamlaka ya nchi.
Hata hivyo, katiba mpya na sheria za uchaguzi zimeibua madai ya kumpendelea katika azma yake ya kuwania urais. Katiba hiyo mpya haikumzuia Nguema kugombea urais, tofauti na ilivyo kwa viongozi wengine wa mpito.
“Baada ya tafakuri ya kina na kwa kujibu maombi yenu mengi, nimeamua kugombea katika uchaguzi wa urais tarehe 12 Aprili 2025,” Nguema aliwaambia wafuasi wake.