
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Consolata Mwasege (47), mfanyabiashara na mkazi wa Ilomba Jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kughushi nyaraka mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo imesema mtuhumiwa alikutwa na nyaraka mbalimbali za kughushi ambazo ni kadi 22 za vitambulisho vya Taifa (NIDA) za watu tofati, kadi nne za mpiga kura zenye majina ya watu tofauti lakini ukiskani QR Code inaonesha jina la mtu mmoja kwenye kadi zote nne.
Zingine ni vipeperushi vya matangazo ya ‘freemason’ 200, na kompyuta moja inayotumika kutengenezea nyaraka hizo za kughushi.
Aidha, taarifa imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akighushi nyaraka hizo kwenye ‘stationery’ iitwayo CO stationary kwa lengo la kujipatia kipato isivyo halali, na kwamba nyaraka hizo zimepelekwa makao makuu ya NIDA Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.