Kisa cha Rais Sankara na rafiki yake Compaoré

0
5

Blaise Compaoré na Thomas Sankara walikuwa marafiki wa karibu. Waliongoza mapinduzi ya mwaka 1983, yakamfanya Sankara kuwa Rais wa Burkina Faso, huku Compaoré akiwa mshirika wake mkuu.

Baada ya miaka minne ya utawala wa Sankara, tofauti kati yao zilianza kuonekana. Sankara alikuwa kiongozi mwenye msimamo mkali dhidi ya ukoloni, ufisadi, na mataifa ya Magharibi, wakati Compaoré aliona sera zake ni kali sana na zenye kuhatarisha mahusiano ya Burkina Faso na mataifa makubwa kama Ufaransa.

Mnamo 15 Oktoba 1987, Compaoré aliongoza mapinduzi yaliyomuondoa Sankara. Wanajeshi waliomuunga mkono Compaoré walimvamia Sankara na wafuasi wake wakawaua kwa risasi. Compaoré alikana kuhusika lakini ushahidi ulionesha kuhusika moja kwa moja katika njama hiyo.

Baada ya kuingia madarakani, Compaoré alifuta sera nyingi za Sankara na kutawala kwa miaka 27.

Oktoba 2014, Compaoré alijaribu kubadili katiba ili kuongeza muda wake wa kutawala, jambo lililozua maandamano makubwa na kupelekea kujiuzulu kisha kukimbilia nchini Ivory Coast.

Mwaka 2022, mahakama ya Burkina Faso ilimhukumu kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya Sankara, ingawa alihukumiwa akiwa uhamishoni nchini Ivory Coast. Sasa Compaoré amepewa uraia nchini humo.