Prof. Kabudi aufuta uongozi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini

0
4

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi ameufuta Uongozi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) baada ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa na wadau wa mchezo wa ngumi.

Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imeeleza kuwa, Mei 08, 2024, Waziri aliunda Kamati Maalum ya uchunguzi yenye jukumu la kuchunguza malalamiko hayo na kubaini ukweli wake.

“Baada ya kamati kukamilisha uchunguzi iliwasilisha taarifa ya yaliyobainika kulingana na tuhuma zilizowasilishwa. Kamati ilijidhihirisha pasi na shaka kuwa uongozi ulikuwa na mapungufu ya kiutendaji,” imesema taarifa.

Kwa mujibu wa Wizara hiyo, mapungufu yaliyobainika ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume na sheria za nchi, katiba ya Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania ya mwaka 2018 pamoja na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na usimamizi wa rasilimali za kamisheni.

Mengine ni matumizi mabaya ya fedha kinyume na sheria za nchi, Katiba ya Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania 2018 pamoja na kanuni za uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za kamisheni.

Kufuatia mapungufu hayo, Waziri Kabudi ameelekeza hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi ya viongozi walioondolewa madarakani, ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wa vyama na mashirikisho na michezo nchini.