TMA yatangaza uwepo wa kimbunga ‘JUDE’ kwenye Bahari ya Hindi

0
6

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza uwepo wa kimbunga ‘JUDE’ katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji.

Katika taarifa iliyotolewa na TMA, imesema uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji mchana wa leo na kupungua nguvu yake, na kwamba kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya Machi 13 hadi 15, 2025.

TMA imesema kutokana na mwelekeo na umbali wake Kimbunga JUDE hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja nchini. Hata hivyo, uwepo wa kimbunga hicho katika eneo la Rasi ya Msumbiji unatarajiwa kuchagiza mifumo ya hali ya hewa nchini na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali.

“Uwepo wa kimbunga hicho unaendana sambamba na kuanza kwa msimu wa mvua za Masika, 2025 katika maeneo yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kama ilivyotabiriwa awali na taarifa kutolewa kwa umma mnamo tarehe 31 Januari 2025,” imesema TMA.

Aidha, TMA imewashauri watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta, na kwamba itaendelea kutoa taarifa juu ya kimbunga hicho.