
Wizara ya Afya imethibitisha uwepo wa wagonjwa wawili wenye maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya imesema ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili, zikiambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo.
“Kati ya wagonjwa hao, mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za afya, imesema inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili wapatiwe matibabu.