Mramba: Biashara ya kuuziana umeme kutainufaisha Tanzania

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu hatua ya Serikali kununua umeme nchini Ethiopitia kupitia nchini Kenya hadi Namanga mkoani Arusha akisema utaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo kwa sasa inatumia umeme unaozalishwa katika mikoa ya Kusini.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Mramba amesema ununuzi wa umeme kutoka nchi jirani haimaanishi kuwa nchi iko katika changamoto ya upungufu wa umeme kwa kuwa mpaka sasa Tanzania inazalisha umeme wa kutosha ambao ni takriban Megawati 3796.
Amefafanua kuwa hatua hiyo ina faida kwa pande zote mbili kwa kuwa njia itakayotumiwa kununua umeme nchini Ethiopia ndio hiyo itakayotumiwa kuuza umeme kwa nchi zenye uhitaji.
Akifafanunua zaidi, amesema jinsi umeme utakavyokuwa ukinunuliwa, umeme wa Ethiopia utaingizwa kwenye mfumo wa Gridi ya Kenya na kisha Kenya itatoa umeme kuja Tanzania ikifidia umeme ulioingizwa kutoka nchini Ethiopia.
‘’Makubaliano haya yako ya pande mbili kuna wakati sisi tutanunua umeme na kuna wakati tutatumia njia hiyo hiyo kuuza umeme kwa nchi jirani, tunavyoangalia hali ya Kaskazini kwa sasa tunaona sisi tutachukua zaidi kuliko kupeleka lakini kuna wakati na wenyewe wanaweza wakahitaji umeme na tutatumia njia hiyo hiyo kuwapelekea” amesema
Ameongeza kuwa kununua na kuuziana umeme kwa nchi si jambo geni na Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikinunua umeme nchini Uganda kwa ajili ya Mkoa wa Kagera, nchini Zambia kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa na nchini Kenya kwa baadhi ya maeneo ya mkoa wa Tanga hususan ya mpakani.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Zambia, ambapo kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa Tanzania kuuza umeme kwa nchi za Kusini mwa Afrika.