
Kufuatia serikali kutangaza uwepo wa ugonjwa wa Mpox nchini, Wizara ya Afya imesema imeanza kutekeleza afua za afya ili kuweza kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo ndani na nje ya nchi ambapo imetoa mwongozo kwa wasafiri utakaoanza kutekelezwa mara moja.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo imesema wasafiri na wafanyakazi wote katika maeneo ya mipakani wanapaswa kuzingatia hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kama unawaji wa mikono, kuacha angalau umbali wa mita moja baina ya mtu mmoja na mwingine na kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa huo kwa kupiga simu namba 199 bure.
Katika maeneo yote ya mipaka (viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari) wasafiri wote watafanyiwa uchunguzi wa awali wa afya ikiwemo kupimwa joto la mwili, na watakaobainika kuwa na homa au vipele watafanyiwa uchunguzi wa kina.
Aidha, Wizara imesema elimu kuhusu utoaji wa taarifa mapema na ushauri wa afya kuhusu kuripoti dalili zozote za ugonjwa huo itatolewa kwa wasafiri wote mipakani, na wote waliotangamana na wagonjwa wa Mpox watashauriwa kufuatilia afya zao na kutoa taarifa katika kituo cha afya kilicho karibu.
Pia imetoa rai kwa wasimamizi na wamiliki wote wa vyombo vya usafiri pamoja na madereva kufuata taratibu za kiafya zikiwemo uchunguzi wa kiafya, ukaguzi wa usafi wa vyombo vya usafiri, kunawa mikono, matumizi ya vitasa mikono na kutoa taarifa mara moja kuhusu msafiri mwenye dalili za ugonjwa huo kwa mamlaka za afya mipakani.