Benki ya Dunia: Rais Samia amekuwa chanzo Tanzania kuongezewa kiwango cha kukopa

0
6

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dkt. Zarau Kibwe, amepongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa ni chanzo cha kuongezeka kwa kiwango cha mkopo ambacho Tanzania inaweza kupata kutoka Benki ya Dunia, kutoka Dola bilioni 5 [TZS trilioni 13] hadi Dola bilioni 12 za Marekani [TZS trilioni 31.7 ].

Dkt. Kibwe ameyasema hayo jijini Washington, Marekani wakati akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyemtembelea ofisini kwake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukutana na wadau wa sekta ya ujenzi na kuhudhuria mikutano ya kimataifa.

Kibwe amesema kuwa hadhi ya Tanzania kimataifa imeimarika, na sasa inatambulika kama moja ya mataifa yanayoendeshwa kwa ufanisi barani Afrika.

“Sijui huko nyumbani kama mnaliona au kulizungumza hili. Katika muda mfupi ambao Rais Samia ameingia madarakani, ukomo wa Tanzania kwenye uhusiano wake na Benki ya Dunia umeongezeka kutoka dola bilioni tano hadi bilioni 12. Hili si jambo la kawaida,” amesema Kibwe.

Kwa upande wake, Waziri Ulega amempongeza Kibwe kwa kushika wadhifa huo mkubwa kama Mtanzania, akisema kuwa Watanzania wanajivunia mafanikio yake. Pia, ametumia fursa hiyo kueleza maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ikiwemo ujenzi wa barabara, mwendokasi na madaraja.

Katika majibu yake, Kibwe amemhakikishia Waziri Ulega kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku akimpongeza kwa msukumo mkubwa katika sekta ya ujenzi.

Send this to a friend