
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limetoa ufafanuzi wa kutekwa kwa mtoto Shadrack Adam (11) mwanafunzi wa darasa la Sita, ambapo limesema kuwa mtoto huyo alitoroka nyumbani kwao Februari 10, 2025 majira ya saa 1 usiku katika Kijiji cha Nanjoka wilayani Tunduru baada ya kuiba shilingi 9000 kwenye jaketi la mama yake.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema baada ya kuiba fedha alipanda basi kuelekea Dar es Salaam na ndipo alipookotwa na msamalia mwema baada ya kumwona akizurura Stendi ya mabasi Mbezi na kumpeleka nyumbani kwake kisha kumhoji, ambapo alidanganya kuwa ametekwa na watu waliokuwa kwenye gari na kumchukua hadi Dar es Salaam.
“Baada ya taarifa hiyo, msamalia mwema huyo alirekodi video fupi na kuisambaza katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya utambuzi wa ndugu wa mtoto huyo, ndipo mama mzazi wa mtoto alipopata taarifa juu ya kupatikana kwa mtoto wake na kuwasiliana na mtoa taarifa kwa ajili ya taratibu za kumrudisha Tunduru,” amesema
Aidha, imesema mama mzazi ameeleza kuwa mtoto huyo hakutekwa bali amekuwa na tabia ya kutoroka nyumbani na hiyo ni mara ya tatu anatoroka “mara ya kwanza alitoroka na kwenda Dar es Salaam, mara ya pili alitoroka kwenda Masasi na hii ni mara ya tatu kutoroka baada ya kuiba fedha.
Jeshi la Polisi limewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Ruvuma juu ya tukio hilo likisema kuwa mtoto huyo amekiri mwenyewe kuwa hakutekwa bali aliiba fedha na kutoroka.