
Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), zimetiliana saini mkataba wa msaada wa Yen za Japan bilioni 1.527 [sawa na shilingi bilioni 27.3] kwa ajili ya kuboresha sekta ya Afya nchini.
Mkataba huo umesainiwa katika Ofisi za Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yoichi Mikami na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Hitoshi Ara, kwa niaba ya Serikali ya Japan.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amesema fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa vifaa-tiba ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.
Dkt. Mwamba amesema ufadhili huo muhimu unaendana na mpango wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao pamoja na masuala mengine, unalenga kutatua changamoto za ubora katika utoaji huduma za afya nchini.
“Ufadhili huu unaunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya afya, zinazolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wakati kwenye jamii,” amesema Dkt. Mwamba.
Naye, Mwakilishi Mkazi wa JICA, Hitoshi Ara amesema JICA imekuwa ikitoa msaada mkubwa katika sekta ya afya ya Tanzania kwa miaka mingi, katika kuimarisha usimamizi wa hospitali na kujenga uwezo wa usimamizi wa ubora wa huduma za afya kupitia mbinu mbalimbali, katika Hospitali za Rufaa za Kanda.