WHO yasema zaidi ya milioni 10 wanaweza kuambukizwa HIV baada ya Marekani kusitisha misaada

0
2

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha uwezekano wa maambukizi mapya ya HIV zaidi ya milioni 10 na vifo vya watu milioni 3, kufuatia kusitishwa kwa msaada wa Marekani unaosaidia upatikanaji wa dawa za HIV.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kusitishwa kwa msaada huo kunaweza kuharibu mafanikio ya miaka 20 yaliyopatikana katika kupambana na HIV.

Pia ameongeza kuwa jitihada za kudhibiti magonjwa mengine kama polio, malaria, na kifua kikuu zimeathirika vibaya.

Marekani kupitia Rais Donald Trump ilitangaza kusitisha kutoa fedha za misaada kupitia miradi iliyokuwa chini ya Shirika lake la misaada la USAID, hali iliyoibua taharuki hasa kwa nchi nyingi za Afrika zinazotegemea fedha za ufadhili kushughulika na magonjwa kama Ukimwi.

Kwa mujibu wa WHO, hatua hiyo imeathiri usambazaji wa dawa katika nchi saba za Afrika, zikiwemo Kenya, Lesotho, Sudan Kusini, Burkina Faso, Mali, Nigeria, na Haiti, ambazo zinaweza kuishiwa dawa ndani ya miezi michache ijayo.

Send this to a friend