
Mwanamke mmoja Mkenya, ambaye kwa sasa yuko gerezani Hong Kong, amedai kuwa aliwahi kufungwa nchini Ghana pamoja na Mkenya anayesubiri kunyongwa nchini Vietnam, Margaret Nduta kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Mwanamke huyo aliyetoa taarifa hiyo kupitia mchungaji wa gereza nchini humo, amesema walilazimishwa na genge la wasafirishaji wa dawa za kulevya lenye makao yake Nigeria, ambalo lilitishia kuua watoto wao na wapendwa wao ikiwa wangekataa kubeba dawa hizo.
Ameongeza kuwa alijisalimisha kwa mamlaka baada ya kulazimishwa kubeba dawa za kulevya na mtandao huo wa Nigeria.
Hata hivyo, familia ya Nduta imekana madai hayo ya kuwahi kufungwa nchini Ghana wakisisitiza kuwa hakuwahi kuondoka Kenya kabla ya safari yake ya kwenda Asia mwaka 2023 kwa ajili ya kazi ya nyumbani.
Mchungaji Wotherspoon ametoa wito kwa serikali ya Kenya kuwasilisha taarifa hizo mpya kwa mamlaka za Vietnam, akisema kwamba kujua kuwa Nduta alilazimishwa kufanya hivyo chini ya vitisho kunaweza kusaidia kuokoa maisha yake.