‘Lipa ChapChap’: Benki ya Exim Yaja na Mapinduzi ya Malipo Kidijitali

Benki ya Exim Tanzania imechukua hatua madhubuti katika kuunda mustakabali wa malipo ya kidijitali kwa kuzindua ‘Lipa ChapChap’, suluhisho la malipo yasiyotumia fedha taslimu linalorahisisha miamala kwa wafanyabiashara na wateja binafsi.
Zaidi ya kuwa huduma mpya, Lipa ChapChap ni hatua muhimu katika dhamira ya benki ya kuendeleza ujumuishi wa kifedha, ubunifu, na uchumi wa kidijitali nchini Tanzania.
Sababu kubwa ya ubunifu huu ni ongezeko la mahitaji ya malipo yasiyotumia fedha taslimu na ujumuishi wa kifedha. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuhamia kwenye uchumi wa kidijitali. Kupitia Lipa ChapChap, Benki ya Exim inaendana na maono ya BoT ya kujenga mfumo wa kifedha ulio jumuishi na wa kisasa zaidi, hatimaye kupunguza utegemezi wa miamala ya fedha taslimu.
Kwa biashara nyingi, hususan biashara ndogo na ya kati (SMEs), mifumo ya kibenki ya zamani mara nyingi huweka vikwazo kama vile gharama kubwa za miamala na upatikanaji mdogo wa miundombinu ya malipo ya kidijitali. Suluhisho hili la malipo linaondoa changamoto hizi kwa kutoa njia salama na isiyo na gharama kwa wafanyabiashara, ikiwaruhusu kupokea malipo kutoka benki zote na mitandao yote ya simu.
Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na Kati wa benki hiyo, Andrew Lyimo alielezea athari chanya ya mpango huu kwa kusema: “’Maliza Kirahisi, Lipa ChapChap’ ni ushuhuda wa dhamira yetu ya kuleta ubunifu na urahisi. Suluhisho hili siyo tu kwamba linaimarisha ufanisi wa malipo, bali pia linakuza ujumuishi wa kifedha kwa kuhudumia biashara zote, ikiwemo SMEs, kwa njia salama, isiyo na gharama, na inayopatikana kwa haraka. Lengo letu ni kuunda mfumo wa uchumi usiotegemea fedha taslimu unaowanufaisha wafanyabiashara na wateja binafsi.”
Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na Kati wa Benki ya Exim, Bw. Andrew Lyimo (katikati) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya inayojulikana kama Lipa Chapchap, suluhisho bunifu la malipo ya kidijitali ambalo linarahisisha miamala kwa biashara na watu binafsi. Kushoto kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano Bw. Stanley Kafu, na Mkuu wa Idara ya Njia Mbadala za Kidijitali, Silas Matoi kutoka benki ya Exim Tanzania. Tukio hili limefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Kwa kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ya simu, suluhisho hili la Benki ya Exim linahakikisha kuwa biashara za kila aina, kutoka kwa wauzaji wadogo mitaani hadi makampuni makubwa, zinapata mfumo wa malipo wa kidijitali ulio salama na wenye ufanisi.
Kuelekea katika uchumi usiotegemea fedha taslimu ni moja ya vipaumbele vikuu vya BoT, ikiwa na malengo ya kuongeza uwazi wa kifedha, kuimarisha ukusanyaji wa kodi, na kuongeza usalama katika miamala. Kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali kama Lipa ChapChap, utegemezi wa fedha taslimu unapunguzwa, hivyo kupunguza hatari za wizi na udanganyifu.
Kwa mjibu wa BoT, miamala ya kidijitali nchini Tanzania imekua kwa kasi, ikichochewa na huduma za fedha za simu na ubunifu katika teknolojia ya kifedha. Huduma hii mpya ya Benki ya Exim inachochea mwenendo huu kwa kuhakikisha mifumo ya kifedha inafanya kazi kwa pamoja, na hivyo kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wigo mpana zaidi.
Naye Mkuu wa Idara ya Njia Mbadala za Kidijitali, Silas Matoi alisisitiza umuhimu wa usalama na ufanisi katika kuhamasisha matumizi, “Usalama ni nguzo kuu ya miamala ya kidijitali, na Lipa ChapChap inatoa uthibitisho wa papo hapo wa miamala, hivyo kuhakikisha wateja na wafanyabiashara wanapata huduma isiyo na wasiwasi. Kwa kuskani tu kupitia simu yako, malipo yanakamilika mara moja—hakuna haja ya kushika fedha taslimu au kadi. Ni salama, rahisi, na imeundwa kwa ajili ya kila mtu.”
Dhamira ya Benki ya Exim ya kuleta mageuzi ya kidijitali haijaishia tu kwa Lipa ChapChap. Benki imeendelea kuzindua bidhaa bunifu zinazolenga kuongeza urahisi wa huduma za kibenki, kuongeza uelewa wa kifedha, na kuwezesha jamii kwa njia za kidijitali. Kwa kutumia teknolojia kutatua changamoto halisi, benki hii inachangia kuunda mustakabali wa sekta ya kifedha nchini Tanzania.
“Kama taasisi ya kifedha inayoangalia mbele, tumejidhatiti kutumia teknolojia kuleta suluhisho bunifu linalojali mahitaji ya wateja,” alisema Stanley Kafu, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano kutoka benki ya Exim. “Lipa ChapChap ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuendesha mabadiliko ya kidijitali na uwezeshaji wa kifedha. Kwa kuondoa vikwazo vya malipo ya kidijitali, hatuleti tu bidhaa mpya—tunaunda mustakabali wa huduma za kifedha.”
Kwa maono yanayolingana na sera za kitaifa na mwenendo wa kidijitali wa kimataifa, Benki ya Exim inajiimarisha kama mshirika muhimu katika mapinduzi ya fedha za kidijitali nchini Tanzania. Hili si tu suluhisho la malipo, bali ni nyenzo yenye nguvu ya kuendeleza ujumuishi wa kifedha, kuongeza ufanisi wa biashara, na kuharakisha safari ya nchi kuelekea uchumi wa kidijitali kamili.
Kadri Tanzania inavyoendelea kuukumbatia ulimwengu wa kidijitali, dhamira ya Benki ya Exim ya kuleta uvumbuzi wa kiteknolojia inahakikisha kwamba watu binafsi na wafanyabiashara wanapata huduma za kifedha kwa urahisi, usalama, na uhakika. Uzinduzi wa Lipa ChapChap ni mwanzo wa sura mpya ya kusisimua katika sekta ya kifedha nchini Tanzania.