Adaiwa kumuua mwanamke kikatili baada ya kumkataa mwaka 2016

0
5

Polisi katika eneo la Bomet Central nchini Kenya wanamshikilia mwanaume mwenye umri wa miaka 28, anayeshukiwa kuhusika katika mauaji ya kikatili ya mwanamke mwenye umri wa miaka 45 kutokana na mgogoro wa kimapenzi.

Mshukiwa, Wesley Cheruiyot Koech, anadaiwa kumuua Rachealine Rutto kikatili ndani ya nyumba yake na kuacha mwili wake ukiwa umetapakaa damu kitandani. Mwili wa marehemu uligunduliwa na binti yake baada ya kumpigia simu siku nzima bila mafanikio.

Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauaji hayo ni kinyongo cha muda mrefu baada ya Rutto kumwacha Koech mwaka 2016, wakati huo, mshukiwa alikuwa na umri wa miaka 19, huku marehemu akiwa na miaka 36. Inadaiwa kuwa Koech alihisi kusalitiwa baada ya kutumia pesa zake na kumwacha.

Kwa mujibu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha makubwa shingoni na majeraha mengi mwilini. Baada ya tukio hilo kuripotiwa kwa polisi, msako mkali ulianza mara moja na Koech alikamatwa akiwa mafichoni katika kijiji cha Sailo, Kipkelion Mashariki.

Mshukiwa alipokamatwa, aliwaongoza maafisa wa upelelezi hadi nyumbani kwake, ambako walikuta ushahidi muhimu, ukiwemo kisu kilichotumiwa kwenye mauaji kikiwa kimefungwa kwenye kitambaa na kikiwa na damu. Pia, pete ya marehemu na simu ya mshukiwa yenye picha za kutisha za mwili wa marehemu zilipatikana.