Polisi: Tunafanya uchunguzi dereva bajaji aliyekutwa ameuawa Arusha

0
7

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limesema linafanya uchunguzi kuhusu tukio la mwili wa Elias Msuya (28) dereva bajaji, mkazi wa Uswahilini Jijini Arusha ambao uligunduliwa ukiwa pembeni ya barabara ya Noah katika mtaa wa Nadosoito, kata ya Terati Jijini Arusha.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salvas Makweli amesema tukio hilo limeripotiwa Aprili 05, 2025 saa 12:30 na kuanza uchunguzi mara moja.

ACP Makweli amebainisha kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikua akiegesha bajaji yake yenye namba za usajili MC 466 DUU maeneo ya Friends corner katika barabara ya Unga ltd – Friends corner kwa ajili ya shughuli za kubeba abiria, na siku ya tukio alikuwa kazini na baadaye mwili wake ulipatikana asubuhi ukiwa umetelekezwa.

Ameendelea kufafanua kuwa walibaini kuwa bajaji aliyokuwa akiitumia marehemu ilikutwa ikiwa imetelekezwa huko katika maeneo ya Enjoro, Kata ya Laroi wilaya ya Arumeru, huku ikiwa imefunguliwa na kuibiwa baadhi ya vifaa.

Aidha amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, na mwili huo umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Muriet kwa ajili ya uchunguzi.

Jeshi la Polisi limetoa rai kwa watumiaji wa vyombo vya moto hasa kwa wanaosafarisha abiria kuchukua tahadhari na kuwa makini kwa abiria wanaowapakia, na endapo watahisi si watu wema watoe taarifa haraka polisi.