Tanzania kupata ufadhili wa TZS trilioni 1.2 kutoka IMF

0
18

Tanzania inatarajiwa kupata ufadhili wa takribani dola milioni 441 [TZS trilioni 1.2] kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kufuatia makubaliano ya awali yaliyofikiwa kati ya wataalamu wa IMF na mamlaka za Tanzania. Fedha hizo zitatolewa baada ya kupitishwa rasmi na Bodi ya Utendaji ya IMF katika wiki zijazo.

Ufadhili huo unajumuisha ukaguzi wa tano chini ya Mpango wa Mikopo ya Muda Mrefu (ECF) pamoja na ukaguzi wa pili wa Mpango wa Uhimilivu na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (RSF). Jumla ya msaada wa kifedha kutoka IMF kupitia mipango hii miwili itafikia zaidi ya dola milioni 1.2.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kiongozi wa ujumbe wa IMF, Nicolas Blancher, uchumi wa Tanzania umeonyesha mwenendo mzuri, ambapo ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 5.5 mwaka 2024, na unatarajiwa kupanda hadi asilimia 6 mwaka 2025. Hali ya mfumuko wa bei pia imesalia chini ya asilimia 5, ambayo ni lengo la Benki Kuu ya Tanzania.

“Uchumi wa Tanzania unaendelea vizuri, ambapo ukuaji halisi wa Pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 5.5 mwaka 2024, na unatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 6 mwaka 2025. Mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.3 mwezi Machi (kwa mwaka mmoja), na bado uko chini ya lengo la asilimia 5 la Benki Kuu ya Tanzania (BoT),” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, pamoja na matarajio chanya, IMF imeonya juu ya hatari zinazoweza kuathiri uchumi, ikiwa ni pamoja na hali ya sintofahamu ya kiuchumi duniani, mizozo ya kijiografia, na kupungua kwa misaada ya maendeleo kutoka nje. Kwa upande wa ndani, uchaguzi mkuu ujao unaweza kuongeza shinikizo la kifedha na kuchelewesha utekelezaji wa mageuzi muhimu.

IMF imesisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia RSF zitasaidia kuimarisha uthabiti wa kiuchumi na kijamii kwa muda mrefu.

Send this to a friend