
Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imetangaza kuwa imefanikiwa kuzuia jaribio kubwa la mapinduzi dhidi ya kiongozi wake, Kapteni Ibrahim Traoré.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana amesema njama hiyo ilihusisha wanajeshi wa sasa na wastaafu, wakishirikiana na makundi ya kigaidi.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wahusika walikuwa wakifanya maandalizi yao kutoka nchi jirani ya Ivory Coast, na walikuwa na lengo la kushambulia Ikulu ya rais wiki iliyopita.
Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya kijeshi ya Burkina Faso kudai njama ya kuangushwa madarakani, huku nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama kutoka kwa makundi yenye msimamo mkali.
Kapteni Ibrahim Traoré aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwezi Septemba 2022, akimuondoa Kanali Paul-Henri Damiba, aliyekuwa ameahidi kurejesha usalama lakini akashindwa kudhibiti mashambulizi ya makundi ya wanamgambo.