Dkt. Mwinyi: Serikali ya Zanzibar itahakikisha Muungano unaendelea kuimarika

0
6

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha Muungano unaimarika na kufikia dhamira ya waasisi ya kudumisha uhuru, umoja na mshikamano kwa Watanzania.

Dkt. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Kutunuku Nishani za Kumbukumbu ya Muungano ilioambatana na Uzinduzi wa Kitabu cha MWALIMU JULIUS NYERERE PHOTOGRAPHIC JOURNEY cha Historia ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Ameeleza Watanzania wana kila sababu ya kudumisha muungano kwani ni tunu ya Taifa ya kujifaharisha nayo, na ni kielelezo cha Muungano wa mafanikio Barani Afrika.

Amesema waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume walikuwa na dhamira thabiti ya kuwaunganisha Watanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo, jambo linalopaswa kudumishwa na kila Mtanzania.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazozitekeleza za kumaliza changamoto za Muungano kupitia vikao vya majadiliano hadi kubakia changamoto tatu kati ya changamoto 25 zilizokuwepo awali.