
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iimarishe na kufanya ufuatiliaji wa watendaji wa vyama vya ushirika ili wazingatie maadili ya utumishi wa ushirika, uwazi, uwajibikaji na utawala bora, na hivyo kuwavutia wanachama na wawekezaji.
Sambamba na hilo, ameiagiza Wizara ya Kilimo, pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, iharakishe na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati yote iliyopitishwa, hususan katika maeneo ya teknolojia ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo, na masoko ya mazao.
Ametoa maagizo hayo leo wakati akizindua mdahalo wa Upatikanaji Mitaji ya Fedha za Maendeleo ya Ushirika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Pia, Waziri Mkuu amezindua ripoti ya Mwaka ya Kilimo kwa mwaka 2022/2023, 2023/2024.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzisisitiza taasisi za kifedha, zikiwemo benki na mifuko ya maendeleo, ziendelee kushirikiana kwa karibu na vyama vya ushirika kwa kuweka mifumo rafiki ya upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Aidha, amewataka wakulima na wananchi kwa ujumla wahakikishe wanajiunga na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa, ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.